My Perspectives

The World is a funny, complex, progressive and regressive place in many ways. My Perspectives is a space where I will be sharing my perspectives of the world. My focus will be on sociopolitical, environmental politics and socio-justice matters. Come, join the discussion!

Edward Lowassa na ‘Mafanikio’ ya UKAWA

Hivi karibuni nilipata nafasi ya kuwa na maongezi tata na ndugu yangu wa karibu kuhusu mafanikio ya UKAWA kwenye uchaguzi uliopita. Katika maongezi yetu, ndugu yangu alinijuza kwamba mafanikio ya UKAWA kupata asilimia 40 ya kura zote zilizopigwa zilitokana na uwepo wa Edward Ngoyayi Lowassa.

Kuna uwezekano kwamba kulikuwepo na mafanikio fulani iliyotokana na ujio wa Edward Lowassa kwenye kambi la upinzani. Ila ikichunguzwa kwa undani zaidi, ujio wa Edward Lowassa haikuinufaisha kambi la upinzani chini ya mwamvuli ya UKAWA  bali iliondoa imani ya wapiga kura na kusababisha UKAWA kutofikisha malengo yake  ya kuutwaa uongozi wa nchi.

Kilichokuwa dhahiri zaidi kwenye uchaguzi uliopita, ni kwamba Watanzania wengi, akiwemo ndugu yangu, walichoshwa na uongozi wa CCM. Kati ya viongozi waliojitosa kugombea ngazi ya juu zaidi ya uongozi nchini, na waliokuwa na sifa za kujadili walikuwa ni wawili tu: John Pombe Magufuli na Edward Ngoyayi Lowassa. Na kwa namna moja au nyingine tunawezasema kwamba wote walikuwa wakitoka CCM. Swali la msingi la kujiuliza ni hili: ikiwa Watanzania walichoshwa na uongozi wa CCM ambao umekuwa ukitoa ahadi hewa kwa wananchi kwa miongo kadhaa, je, wangemwamini Edward Lowassa ambaye ana sifa ya hujuma ya uchumi ya taifa na utumiaji mbaya wa madaraka hata kama alikuwa anagombea Urais kwa tiketi ya UKAWA?

Kwa kuanzia, ni vyema kusema bila kusita kwamba ingawa Lowassa aliwavutia watu wengi sana tangu alipotangaza kuungana na CHADEMA/UKAWA hakuwa chanzo cha mafanikio ya UKAWA kupata asilimia 40 za kura kwenye uchaguzi uliopita. Kabla ya mtu yeyote kusema kwamba Lowassa alileta mafanikio UKAWA, sharti ikumbukwe kwamba UKAWA ni au ilikuwa umoja wa vyama mbali mbali za siasa uliojitokeza kama vuguvugu wakati wa mchakato wa katiba mpya. Pili, lazima kuwepo na tathmini na uchambuzi kujua asilimia gani ya wapiga kura walitoka kwenye chama gani.

Kipengele cha kwanza ni rahisi kusuluhisha. Asilimia 40 ya kura zilizopigiwa UKAWA ilitokana na wanachama na wapiga kura tofauti waliokuwa wakiunga mkono vyama shiriki chini ya mwamvuli ya UKAWA. Kipengele cha pili itakuwa vigumu maana kura ni siri na ni vigumu kujua ni wangapi walipigia kura NCCR-Mageuzi, CUF, CHADEMA au vyama shiriki kwenye umoja huo – UKAWA.

Siasa Nchini Tanzania

Ukiangalia hali ya hewa katika ulingo wa siasa nchini Tanzania, ni dhahiri kwamba wananchi wanahaha kumpata kiongozi mchapa kazi na mwenye utashi wa kisiasa. Kwa lugha ya kawaida, utashi wa kisiasa ni mtu – mwanasiasa kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi magumu. Kwa kuwa hitaji hili liko wazi kwa wanasiasa, na limekuwepo kwa muda mrefu: kila kiongozi anakuja na kauli mbiu inayolenga kumridhidha mwananchi wa kawaida.

Tukiangalia vipaumbele na kaulimbiu kwenye kampeni za chaguzi zilizopita, zote zililenga kumfurahisha mwananchi wa kawaida, japo kwa kipindi cha kampeni. Hebu tuangalie vichache: kwa Mkapa ilikuwa kuwaunganisha Watanzania na dunia kwa njia ya utandawazi kijamii, kimaendeleo na kiteknolojia. Kwa Kikwete ilikuwa kuleta “maisha bora kwa kila mtanzania”. Na kwenye uchaguzi uliopita: ahadi ya kuwajibika na kuwajibishwa kwa watendaji serikalini kwa kauli mbiu “hapa kazi tu” ya John Pombe Magufuli. Kama ishara ya awali kuhakikisha kwamba wananchi wanaona kwamba Rais Magufuli siyo muongo kama marais waliomtangulia, ameanza kazi kwa kasi isiyo ya kawaida.

Ingawa kasi hii siyo ya kawaida, na ingawa Rais wa awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete aliangua kicheko alipokuwa anamshabikia Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kuhakikisha kwamba mashine ya kuchunguza magonjwa mbali mbali mwilini (MRI), Watanzania wengi wanafurahi. Furaha yao si kwa sababu Rais Magufuli ni kiongozi mzuri.

Furaha yao ilisababishwa na matokeo, japo ya muda mfupi, ya ziara ya ghafla ya Rais Magufuli kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili. Kama msomaji upo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, ni lazima ulipata kuona ilani mbali mbali kuonya wananchi wanaopita karibu na hospitali ya taifa ya Muhimbili kuhusu tukio ya wapita njia au waliokwenda kutembelea wagonjwa kupimwa na madaktari hospitalini humo. Tunapotafakari matukio kama haya, ni lazima tukumbuke kigezo kimoja cha msingi: Watanzania wana hamu ya kumpata kiongozi anayejali maslahi ya wananchi. Kwa hiyo, kwa Mtanzania wa kawaida, mwanasiasa na kiongozi yeyote anayeongea lugha inayoleta picha ya kutofumbia macho maovu atashabikiwa na kuungwa mkono na wananchi.

Edward Lowassa, CCM na UKAWA

Tukubali kwanza kwamba Edward Lowassa ni mwanasiasa mkongwe na maaarufu sana nchini Tanzania. Umaarufu wa Lowassa unatokana, miongoni mwa sababu zingine, amekuwa katika siasa kwa muda mrefu. Kingine ni kwamba, na kwa maoni ya umma, kukubali kuhusika kwenye sakata la kampuni hewa ya ufuaji wa nishati ya umeme – Richmond iliyoipelekea nchi kupata hasara kiasi cha bilioni 240 hela za kitanzania ambayo ni sawa na dola za kimarekani milioni 120 kwa mwaka 2008.

Kwa kukabidhi barua yake ya kujiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu wa Tanzania japo kwa shingo upande, alikonga nyoyo za Watanzania kuwa kiongozi anayeweza kufanya maamuzi magumu. Hata ikimaanisha kukubali kosa na kuachia wadhifa wake serikalini.

Sifa kama hiyo haikuwahi kuoneshwa na kiongozi yeyote yule hapa nchini Tanzania . Ikumbukwe kwamba alipojiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu, Lowassa alikuwa na kikao na Rais Kikwete na kulikuwa na makubaliano. Haya yote yamenakiliwa kwenye hansadi ya kikao cha dharura Bungeni tarehe 7/2/2008 iliyofanyika alipojiuzulu wadhifa huo pamoja na waziri wa Nishati na Madini kwa wakati huo Nizar Karamagi na naibu wake Ibrahim Msabaha. Kwa kawaida, wengi wa watumishi serikalini mara kwa mara wanapewa uhamisho kutoka kwenye wizara au idara moja kwenda ingine ikitokea kashfa. Kwa hiyo Lowassa alikuwa na wenzake walikuwa mfano.

Ila inabidi tujiulize, je, Lowassa alipojihusisha na sakata la Richmond, alikuwa kwenye serikali ipi? Jibu ni la wazi! Alikuwa CCM na uongozi wa CCM haikumwajibisha Lowassa na washirika wake kwa kuwachukulia hatua za kisheria. Mwananchi au mfanyabiashara wa kawaida ambaye hakuwa na faida yoyote kwa serikali angepelekwa mahakamani mara moja na kufunguliwa kesi na kuhukumiwa kifungo. Lakini hili halikufanyika kwa Lowassa wala Karamagi au Msabaha.

Alipopokelewa Edward Lowassa UKAWA, hatuwezi kusema kwamba wana-UKAWA hawakujua hayo yote. Bali kuna sababu chache za kubashiri juu ya maamuzi ya UKAWA kumtawaza Lowassa: nazo ni, umaarufu wa Lowassa kisiasa, hela alizo nazo, na maoni ya umma kwamba Lowassa ana uwezo wa kufanya maamuzi makubwa. Tunadiriki kusema pia kwamba UKAWA ilimkaribisha Lowasa kuikebei CCM na pia kutaka kuingia madarakani kwa njia ya mkato.

Edward Lowassa, UKAWA na Uchaguzi Mkuu 2015

Watanzania wengi tumeshuhudia kwamba Karamagi na Msabaha wamekuwa kimya tangu walipojiuzulu kutokana na sakata la Richmond mwaka 2008. Ila Edward Lowassa ameendelea na siasa na kuwa sauti ya kusikilizwa ndani ya CCM na hivi karibuni, ndani ya UKAWA. Kwa Watanzania walio wengi, Lowassa angesaidia kuling’oa CCM kutoka madarakani.

Wengi inaonekana waliamini hivyo bila kujiuliza ni madhara gani yataweza kutokea kwa kuzingatia kwamba Lowassa ni CCM damu? Je, Lowassa alitumwa na CCM kuhakikisha kwamba wananchi hawawi na imani na UKAWA kwa kumkubali Lowassa ghafla bin vuu? Kwa namna nyingine, je, Lowassa alikubali kutolewa kafara mara ya pili kukiokoa chama chake – CCM? Matokeo yanaonesha wazi kwamba CHADEMA na washirika wa UKAWA walijipiga risasi miguuni kwa kumtawaza   Edward Lowassa. Na matokeo ya uchaguzi wa urais unathibitisha kwamba uteuzi wa Lowassa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya UKAWA ilikuwa kosa kubwa kwa upande wa uongozi wa UKAWA. Na kwa upande mwingine, kama hii ilikuwa mkakati wa CCM kushinda uchaguzi mkuu 2015, basi ni Dhahiri kwamba walifanya kazi nzuri. Walifaulu.

Hivyo basi, tukiangalia matokeo ya uchaguzi mkuu 2015, tunaweza kusema kwamba Edward Lowasa badala ya kuwa dili UKAWA, inaonekana wazi wazi kwamba alileta hasara, aibu na kuonesha kwamba vyama vya upinzani Tanzania, hasa zile zinazounda UKAWA hawajakuwa kisiasa kujua nani anayefaa kwenye nafasi ipi na kwa wakati gani,

Wakati tukiendelea kutathmini madhaifu na mema ya wanasiasa na vyama vya siasa nchini Tanzania, ni jambo jema na yenye busara tukatafakari ni wapi tulikotoka, tulipo na tunakoelekea kisiasa. Itakuwa jambo la busara pia kujiuliza maswali haya: ahadi zipi zilitolewa au makubaliano yapi yalifikiwa kati ya Lowassa na rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipojiuzulu uWaziri Mkuu? Je, alipojiengua uanachama CCM, ni siri zipi CCM iliogopa kwamba labda zingewekwa wazi iwapo Lowassa angepata urais kupitia UKAWA? Je, ni kwa sababu gani hadi sasa hivi, Lowassa hajibu chanzo chake kuondoka CCM na kujiunga na vyama vya upinzani?

Haya yote na maswali mengine mengi yanabaki kuwa maswali tata na yanayohitaji majibu. Watanzania tunapaswa kutafakari na kujiuliza maswali haya japo kwa kuvutia majadiliano juu ya mwelekeo wa siasa na mwenendo wa wanasiasa na ushiriki wa wananchi kuhakikisha uwepo wa siasa endelevu na shirikishi.

Log In

%d bloggers like this: