My Perspectives

The World is a funny, complex, progressive and regressive place in many ways. My Perspectives is a space where I will be sharing my perspectives of the world. My focus will be on sociopolitical, environmental politics and socio-justice matters. Come, join the discussion!

‘Siasa Endelevu’: Ni Jukumu la Nani?

JP Magufuli

John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kwa muda mrefu sasa, Watanzania wamejijengea hulka ya uhasimu wa kisiasa. Kila mwanasiasa amejifunga kimawazo, kisiasa na kifalsafa kwenye sera na imani ya vyama vyao. Hali hii siyo ya ajabu. Cha ajabu kwenye hali hii ni pale wanasiasa wanapojifunga kimawazo na kufumbia macho maovu yanayotendeka ndani ya chama chao – na uongozi wa nchi. Hii hali imetupelekea kupotoka kisiasa na kutufanya kukosa nafasi ya kuona wazo mbadala kutoka kwenye kambi ya siasa iliyo na mtazamo tofauti na kile kinachoangazwa na kupigiwa debe kwenye vyama vyetu. Hii siyo siasa endelevu.

Tanzania imempata Rais mwingine. Ingawa ni mtu tofauti na mwenye sifa tofauti, anatoka kwenye chama ambacho kimeongoza nchi kwa muda mrefu sana – Chama Cha Mapinduzi. Kwa Watanzania walio wengi, hasa hasa wale ambao wanaamini kwenye uongozi wa chama kimoja, CCM kutwaa uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni tukio la kujivunia. Wala siyo ishara kwamba kutwaa uongozi wa nchi ni kutwaa jukumu nzito kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Ila kwa tafakari, wakati huu na karne tunamoishi siyo karne ya kujitukuza kupata ushindi. Siyo wakati wa kujisifia kuwa mwenye uelewa zaidi. Wala siyo karne ya kujisusha na kufikiri kwamba mawazo yako, ukiwa mwanasiasa au mwananchi wa kawaida, hayana maana. Bali ni wakati wa kuipa uzito jukumu la kila mmoja wetu. Ni wakati wa kuhakikisha kwamba uongozi uliopo madarakani, ingawa wengi bado wana huzuni, unawajibishwa. Huu ni wasaa wa kuuliza na kujiuliza maswali magumu. Pia ni wakati wa kuhakikisha kwamba tunachukua nafazi zetu kizalendo kuitumikia nchi yetu katika nafasi zetu. Nafasi hizi siyo lazima ziwe ofisini au Bungeni bali kweye shughuli zetu za kila siku. Ingawa kwa ugumu na changamoto za maisha.

Lazima kila Mtanzania wakiwemo watakaoiongoza nchi kwa miaka 5 ijayo kuuliza maswali kama yafuatayo: Je, ni nini tatizo kuu linaloikumba nchi yetu Tanzania? Je, ni jukumu la nani kuhakikisha nchi inakabili changamoto za kijamii, kiuchumi na kimazingira bila kusua? Swali lingine ambalo nafikiri itabidi tujiulize bila haya, ni: Ni nani aliye na jukumu kubwa zaidi kuhakikisha kwamba changamoto za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimazingira zinakabiliwa na kurejesha Tanzania kwenye ubora wake na kumiliki uzalendo wetu tena?

Baada ya kusema hayo, naomba nirejee kwenye andiko langu leo asubuhi hapa mtandaoni na kwenye ukuta wangu wa Facebook. Nilisema kwamba “Ninataka Rais John Pombe Magufuli aniteuwe kuwa Waziri wa Nishati na Madini. ‘Kichaa’ mwenzake! Yeye alikuwa tinga tinga wa bara bara na ujenzi, mie nitakuwa buldozer wa hawa washenzi wanaoilawiti nchi yetu kijamii, kiuchumi na kimazingira!”

Wengi wenu mliposoma andiko hilo, mliunga mkono hoja na kwa kiasi kikubwa ninashukuru kwamba Watanzania tumefikia sehemu tujadiliana maswala ya siasa bila uoga. Nilipoweka andiko hilo, nilikuwa kwenye muda wangu wa kutafakari Siasa nchini kwangu/kwetu Tanzania. Kwa muda mrefu mawaziri na manaibu waziri huwa wanateuliwa kutoka kwenye chama tawala. Hili linafanyika kwa imani kwamba kwa kuwaweka makada wa chama tawala katika nafasi hizo, sera ya uchaguzi itatekelezwa. Desturi hii imekuwa kawaida na wengi wanaamini kwamba ni haki ya wanachama wa chama tawala kupewa nafasi hizi.

Kwa mtazamo mpana, hali hii imekuwa ni mmoja wapo ya vikwazo vinavyozuia na kudumaza ubunifu na utashi miongoni mwa watawala wetu. Wengi wao wanaishia kuwa wazembe. Nafikiri wengi wenu mmeshuhudia mawaziri wetu pamoja na wawakilishi wetu Bungeni kutokuwa na michango chanya kwenye majadiliano ya msingi kisera au kimaendeleo. Kwa ujumla, wanajua kwamba hakuna atakayewawajibisha. Wakifanya kosa kwenye wizara au idara moja, watapewa uhamisho kwenye wizara au idara ingine. Kwa hiyo wanasiasa wetu wanaingia Bungeni na kwenye ofisi zao wizarani kwa ajili ya kupata posho na mishahara. Wachache sana wanawajibika.

Kusema kwangu kwamba “ninamtaka John Pombe Magufuli kuniteuwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini”, ilikuwa inalenga kuona kama tumefika sehemu, katika uelewa wetu kisiasakuona kwamba nafasi za Wizarani na idara zake, ziwe nafasi zitakazokaliwa au kuongozwa na Watanzania wenye uwezo wa kufanya hizo kazi kitaaluma zaidi. Kwa namna ingine, nafasi hizo ziwe nafasi za ajira. Mwajiriwa akifanya kosa, awajibishwe kisheria ikiwemo kupoteza ajira. Nafasi hizo zisiwe zawadi ya kupewa mtu kwa sababu mwanasiasa huyu au kada wa chama yule alikuwa mstari wa mbele kuipigia chama tawala debe wakati wa kampeni. Au kusema kwamba huyu mwanachama amekuwa kwenye chama kwa muda mrefu kwa hivyo anastahiki nafasi hiyo. Kubebana siyo siasa, bali ni upendeleo wa kisiasa na hujuma kimaendeleo kwa nchi na wananchi wake.

Swali lingine la kujiuliza ni hili: je, Rais mpya wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, #JohnPombeMagufuli angeamua kumteuwa mwanasiasa kutoka kwenye chama pinzani kuwa kwenye jopo lake la mawaziri, angekosea? Je, angeamua kwamba nafasi za uwaziri na wakuu wa idara mbali mbali wataajiriwa kitaaluma na kulingana na uzoefu walio nao badala ya kuwa mwanachama wa CCM ingeleta au kupunguza chachu ya ubunifu na utashi kwenye utendaji wa wizara na idara idara zake? Je, hatua kama hii ingekuwa na mchango gani kwenye suala zima la demokrasia? Maswali haya lazima kila mmoja wetu tujiulize na kutafakari.

Kwa kuhitimisha andiko hili, naomba niseme kwamba kukua kijamii, kisiasa na kiuchumi kunahitajika mitazamo mipana na isyofungamana na imani, sera na kauli mbiu ya chama chochote cha siasa. Pamoja na mitazamo mipana, ni sharti tuhakikishe kwamba sera zetu za maendeleo na ustawi wa jamii yetu ya Kitanzania zinazingatia kwamba maendeleo ya kweli haiji kwa kujifunga kwenye imani kwamba, chama hiki cha siasa kikiwa kwenye uongozi, ni sharti wafuasi wake tu ndiyo wapate nafasi za utawala na utendaji. Karne yetu siyo karne ya juzi. Kwa hiyo ni lazima tuweke tofauti zetu za kisiasa pembeni baada ya kampeni na uchaguzi kumalizika na kujiwajibisha wote kama Watanzania kulijenga taifa letu.

Wakati huu basi, ni wakati wa chama tawala, vyama vya upinzani na wale wenye mitazamo tofauti kisiasa kuanza kufanya uchambuzi ya utendaji wa sera za uchaguzi wa chama tawala. Ni wakati pia wa kukosoa mwenendo wa chama tawala kiutendaji, iwapo kutakuwa na mapungufu katika kutimiza ahadi walizotoa. Lengo kuu likiwa kujenga Tanzania imara kijamii, kiuchumi na yenye mazingira masafi kwa wananchi wake.

Information

This entry was posted on Nov 6, 2015 by in Politics & Democracy, The Society.

Log In

%d bloggers like this: